SIKU moja baada ya mnajimu maarufu, Barani Afrika, Sheikh Yahya Hussein kubashiri kuwa mtu atakayejitokeza kushindana na Rais Kikwete kwa ajili ya urais awamu ya pili mwakani atakufa ghafla watoto yatima wa kituo cha Tosamanganga Iringa wametuma salama za Krismas na mwaka mpya kwa Rais Kikwete huku wakimwombea mafanikio makubwa katika uchaguzi mkuu mwaka 2010.
Watoto hao zaidi ya 200 waliopo kituoni hapo walituma salama hizo leo mbele ya katibu tawala wa mkoa wa Iringa Getrude Mpaka wakati wakipokea msaada wa chakula kwa ajili ya sikukuu ya Krismas na Mwaka mpya uliotolewa na Rais Kikwete kwa watoto wa kituo hicho.
Katika risala yao iliyosomwa na mkuu wa kituo hicho Sista Helena Kihwele watoto hao walisema kuwa mbali ya kumpongeza Rais Kikwete kwa upendo wao kwao kwa kuwakumbuka kwa chakula hicho ila bado wao wanapenda kutoa zawadi kwake ya maombi zaidi ili kuhakikisha mwaka 2010 unakuwa ni mwaka wa mafanikio makubwa kwake na Taifa zima la Tanzania .
“Mheshimiwa Rais kweli tunashukuru kwa kutukumbuka watoto yatima wa kituo cha Tosamanganga Iringa kwani wapo yatima wengi sana nchini na vituo vipo vingi ila umetuona sisi….tunaamini umeongozwa na Mungu na sisi tunapenda kutoa shukrani zetu kwa salam za heri ya krismasi na mwaka mpya kwa zawadi ulizotoa ….na zawadi yetu kwako ni kuendelea kukuombea mafanikio mema mwaka 2010…tunakupa ahadi ya msaada was ala zetu kwako”
Walisema kuwa wamelazimika kufanya hivyo ili kumwezesha kuwa na afya njema na kutenda shughuli zake kwa Taifa kwa nguvu ya Mungu .
Pamoja na kupongeza na zawadi hiyo ya sikukuu kwa Rais Kikwete pia walisema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ya vijana wakubwa wanaoruhusiwa kutoka kituoni hapo kurudi kuomba msaada wa elimu kituoni hapo jambo ambalo wanaomba serikali kutoa msaada kwa vijana hao wa kielimu na miradi ya kimaendeleo zaidi.
Kituo hicho kina jumla ya watoto 479 huku watoto 253 wanaishi kituoni hapo na watoto 226 wanapewa misaada wakiwa majumbani kwao.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Rais Kikwete katibu tawala wa mkoa wa Iringa Mpaka alisema kuwa Rais amewatakia watoto hao fanaka kwa Krismasi na mwaka mpya wa 2010 .
Alisema kuwa Rais amefarijika sana kushiriki na watoto hao katika kusherekea sikukuu hizo mbili ikiwemo ya Krismasi ambayo inasherekewa kesho kote duniani na ile ya Mwaka mpya na kuwa kwa upande wake alipenda kufika kula na watoto hao kama njia ya kudumisha upendo kwao
Hata hivyo kutokana na sababu zisizo zuilika amelazimika kutoa zawadi ya chakula chenye thamani ya zaidi ya shilingi 607,000 kwa ajili ya kuungana na watoto hao katika sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya.
Mmiliki wa Blog hii anapenda kuungana na wakristo wote ulimwenguni katika kusherekea sikuu ya Krismasi na Mwaka mpya pia kwa watanzania tuige mfano wa Rais Kikwete kula na Yatima