
SAKATA la mzee huyo pichani wa kijiji cha Ngonalamafuta kata ya Ilalinyi Njombe mkoani Iringa kutekwa na watu waliojifanya askari polisi limeendelea kuchukua sura mpya baada ya polisi kufuta RB ya kwanza na kutoa RB ya kweli kwa walalamikaji huku watu watano wakiongozwa na mzee wa miaka 73 kutiwa mbaroni kwa kuhusishwa kumteka mzee huyo .
Mbali ya polisi kuwashikilia watu hao ambao wanadaiwa kujipeleka wenyewe kituo cha polisi Njombe gari dogo (Tax) ambalo lilitumika kumteka mzee huyo Richard Lipambile (70) siku ya Desemba 23 mwaka jana majira ya usiku ilifika kwa mara nyingine kijijini hapa na kuegeshwa katika nyumba za baada ya watuhumiwa .
Hata hivyo imeelezwa kuwa watuhumiwa wote waliokamatwa ni wa familia moja na ni ndugu na mzee huyo aliyetekwa. Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mtoto wa mzee huyo Aman Chaula alisema kuwa pamoja na kutoa taarifa polisi Njombe kuhusiana na gari hilo ambalo lilitumika kumteka baba yake kuonekana kijijini hapo majira ya saa 6 usiku bado polisi walishindwa kufika kulikamata gari hilo hadi linaondoka kijijini hapo.
Alisema kuwa gari hilo likiwa na watu zaidi na mmoja ndani yake lilionekana kijiji hapo Januari 7 majira ya saa 6 usiku huku likiwa halina namba za usajili mbele wala nyuma.
"Baada ya kuliona gari hili tulipiga simu polisi, polisi walitueleza kuwa wangeweza kufika ili kulikamata gari hilo ila katika hali ya kushangaza hadi gari hilo linaondoka kijijini hapo baada ya kuwepo kwa zaidi ya masaa matatu...hakuna askari aliyefika wala kiongozi wa kijiji ..."
Hata hivyo alisema kuwa gari hilo lilikuwa limeegeshwa katika nyumba ya mmoja kati ya watuhumiwa hao na baada ya kutoka katika nyumba hiyo lilielekea katika nyumba nyingine ya mtuhumiwa moja wapo kabla ya kuondoka kuelekea uelekeo ambao walikwenda siku alipotekwa baba yao.
Hata hivyo aliitaja namba ya RB ambayo wamepewa kwa ajili ya taarifa ya kutekwa kwa baba yao kuwa ni NJ/RB/66/2009 ambayo ni tofauti na ile ya kwanza iliyokuwa ikisomeka No.23/09 .
Chaula alisema kuwa hadi sasa ni siku ya 23 toka baba yao bado hajapatikana toka siku aliyotekwa na watu hao waliojifanya askari polisi wakiwa na mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho Samson Mdembe(70) ambaye alikamatwa na polisi na kuachiwa .
Hata hivyo mtoto ndugu hao wanasifu jitihada kubwa za mtandao wa www.francisgodwin.blogspot,gazeti la Tanzania Daima na kituo cha Radio Ebony Fm kwa kazi nzuri ya kusaidia kumtafuta baba yao na kusaidia kuondoa usumbufu mkubwa ambao polisi Njombe walikuwa wakionyesha kwao ambao kwa sasa toka vyombo hivyo vionyeshe kulishupalia polisi wamekuwa waklifanya kazi kwa kufuata maadili yao
"Kweli vyombo vya habari vinanguvu kwani baada ya kutoka katika mtandao na Radio Ebony Fm kupitia mtangazaji wake Raymond Francis na wenzake akina Juliani na Rose kweli hata polisi walionekana kuanza kutuogopa kuwa tuna mtandao mkubwa wa habari hata ile tabia ya kusema tukodi gari haipo tena zaidi ya baada ya askari kutusaidia vizuri .... kweli Radio Ebony na mtandao wa Bw Godwin vidumu na sio Radio nyingine zinatoa habari za zamani na semina pekee"
Aliomba kwa yeyote mwenye taarifa za mzee huyo ama watuhumiwa anaweza kuwasiliana na ndugu wa mzee huyo Bw Aman Chaula kwa simu namba 0765331702/0753254809
Watu waliokamatwa na polisi wilaya ya Njombe kwa tuhuma za kumteka nyara mzee huyo ni pamoja na Marko Chaula(39) Philimon Chaula (34),Ernesto Chaula(42)Stanle Chaula na mzee Said Matatala(73)ambaye ni baba yao mkubwa na ndugu wa mzee Lipambile ambaye alitekwa.
kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa (ACP) Evarist Mangalla (pichani)amelithibitishia gazeti hili kwa njia ya simu kuhusiana na kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kuwa upelelezi zaidi pamoja na jitihada za kumsaka mzee huyo na watekaji wengine zinafanywa la polisi na kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano wa kumpata mzee huyo na watuhumiwa wengine.
Mzee huyo Lipambile alitekwa usiku wa Desemba 23 mwaka jana na watu zaidi ya watano waliofika kijijini hapo na kujifanya ni askari polisi wa kituo cha Njombe ambao wametumwa kumkamata mzee huyo kwa kuhusisha na kesi iliyofunguliwa kituo cha Njombe dhidi ya mtoto wake wa Dodoma ambaye alifanya uharifu huko.