TIMU zazidi kukamiana kuwania zawadi ya shilingi milioni 5 ya Voda Com katika mashindano ya kombe la Muungano Mufindi ambayo yamezidi kuwa na msisimko mkubwa na kupelekea timu zilizokuwa zikipewa nafasi kubwa ya kushinda kama wenyeji Igowole na Silver Star na Donbosco kubanwa mbavu na kutolewa katika mashindano hayo .
Huku timu ya benki ya wananchi Mufindi (MuCoba) na watani wao wa jadi timu ya Nyamalala sekondari zote za mjini Mafinga kucheza mchezo wa marudiano kesho jumatatu ili kupata mshindi baada ya kugongana matokeo.
Mratibu wa kombe la Muungano Mufindi Daud Yassin ameueleza mtandao huu kuwa mashindano hayo kwa mwaka huu yamekuwa na msisimko mkubwa ukilinganisha na miaka yote iliyopita kutokana timu kucheza kwa kujituma na nidhamu ya hali ya juu kama njia ya kuwania ubingwa huo wa Voda Com Muungano Cup 2010 ambapo mshindi ataibuka na kombe pamoja na fedha taslimu shilingi milioni 5 tofauti na mwaka jana ambapo mshindi alizawadiwa kombe na shilingi milioni 3 toka Voda com.
Aidha Yassin alisema hali ya mashabiki katika wiwanja kwa mwaka huu imekuwa ya kuvutia na kuwa kila mchezo unapochezwa iwe kituo cha Igowole ama shule ya Msingi Wambi mjini Mafinga wananchi wamekuwa wakiacha shughuli zao na kufika katika viwanja hivyo.
Yassin alisema katika mashindano hayo ambapo timu 10 zinashiriki kwa upande wa bara kutoka mkoa wa Mbeya,Rukwa,Ruvuma na Iringa timu za mkoa wa Iringa ambazo zilianza mashindano hayo jumamosi iliyopita baada ya kufunguliwa na waziri wa nchi ofisi ya waziri kiongozi (SMZ) Hamza Hasan Juma katika viwanja wa shule ya msingi Igowole ,timu hizo zimeendelea kufanya vizuri na zile zilizoshindwa zimeaga mashindano hayo.
Akielezea matokeo toka mwanzo wa mashindano hayo alisema kuwa katika mchezo wa ufunguzi Mucoba na Nyamalala zilitoka suluhu ya bila kufungana huku Don Bosco ikiiadhibu Igowole kwa jumla ya goli 2-1.
Wakati mchezo uliofuata MUcoba iliichapa Silver ya mjini Iringa goli 2-0 sanjari na Nyamalala sekondari iliyoifunga timu hiyo ya Silver Stars 2-0 huku Igowole ikiifunga Kitwiru stars 2-1
Mratibu huyo alisema kuwa hadi sasa michezo sita imemalizika huku Nyamalala Sekondari na Mucoba zitacheza mchezo wa marudiano ili kumpata mshindi baada ya kulingana pointi na magoli
Hata hivyo alisema mara baada ya kupata mshindi wa kituo cha Igowole na Mafinga zoezi litakalofuata ni mchezo wa kumpata bingwa wa jumla katika kituo cha Igowole na Mafinga kabla ya kumtafuta bingwa wa jumla upande wa Tanzania bara atakayecheza na bingwa wa Visiwani.
Hata hivyo alisema ufunguzi wa kituo cha Mbarali Mbeya unataraji kufanyia mwanzo mwa mwezi ujao katika viwanja wa Chimala Mbeya .
MWISHO